20 Mei 2023 - 14:12
Duru za Kizayuni zakiri ushindi mkubwa wa Rais Bashar al Assad wa Syria

Duru za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel zimekiri kwamba Rais Bashar al Assad wa Syria amepata ushindi mkubwa kwa kushiriki kwake katika Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League mjini Jeddah na kuonana kwake na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman.

Kikao cha wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilifanyika jana Ijumaa, tarehe 19 Mei mjini Jeddah Saudi Arabia na kuhudhuriwa pia na Rais Bashar al Assad wa Syria ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu uliposimamishwa uanachama wa Damascus kwenye jumuiya hiyo, miaka 12 iliyopita.

Televisheni ya Al Mayadeen imeripoti leo Jumamosi kwamba, duru za habari za Wazayuni zimesambaza picha inayomuonesha Rais Bashar al Assad akipeana mikono na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman  na kuandika: Kinachoendelea hivi sasa ni "ushindi mkubwa wa Syria na kiongozi wake asiye na mpinzani."

Duru hizo za Kizayuni zimedai pia kuwa, sentesi sahihi ya kusema hapa ni kwamba, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ndiyo iliyorejea kwa Syria, si kinyume chake.

Mwandishi mmoja Mzayuni amesema, kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuna maana ya kumalizika rasmi "msimu wa machipuo" wa nchi za Kiarabu na hivi sasa ulimwengu wa Kiarabu umerejea kwenye kilele cha kuguswa na kuwa na wasiwasi na kadhia ya Palestina.

Ni vyema kusema hapa kwamba, Rais Bashar al Assad wa Syria alihutubia kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu mjini Jeddah Saudia, ikiwa ni mara ya kwanza kwake kufanya hivyo tangu Syria iliposimamishiwa uanachama wa Arab League zaidi ya muongo mmoja nyuma. Hotuba hiyo imewahamakisha mno Wazayuni na maadui wa umoja na mshikamano katika safu za Waarabu na Waislamu.

342/